Highlights

Gachagua asema atawania urais katika uchaguzi wa mwaka 2027

Na JB Nateleng

Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, amesema bado anastahili kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 licha ya Mahakama Kuu kuthibitisha kuondolewa kwake madarakani.

Akizungumza Jumanne, siku moja tu baada ya uamuzi huo wa mahakama, Gachagua amepuuza madai kuwa hukumu hiyo imemzuia kuwania wadhifa wowote wa kuchaguliwa, akisisitiza kuwa mchakato wa kisheria bado haujakamilika.

Ameeleza kuwa katiba inatoa nafasi ya kukata rufaa na kwamba hakuna mtu anayepaswa kuzuiwa kugombea uchaguzi kabla ya taratibu zote za kisheria kukamilishwa.

Gachagua amesema ataendelea kutumia njia za kisheria kutetea haki zake huku akidumisha azma yake ya kushiriki katika siasa za taifa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

Gachagua, amepuuzilia mbali fidia ya shilingi milioni 50 aliyopewa na Mahakama Kuu kufuatia kesi iliyohusiana na kuondolewa kwake madarakani akisema kuwa kiwango hicho cha fidia hakilingani na uzito wa ukiukaji wa haki na uhuru wake wa kikatiba aliokumbana nao wakati wa mchakato wa kumwondoa afisini.

Gachagua ametangaza kwamba atajiondoa kwenye mikutano ya kisiasa ya umma kwa siku 45 zijazo na badala yake atajikita katika makazi yake ya Wamunyoro.

Post Comment