Highlights

Kamishna Kamande aonya dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kufuatia wizi wa mifugo Laisamis

Na Samuel Kosgei

Idadi isiyojulikana ya mifugo imeibwa katika eneo la Gudas, Loglogo, eneo bunge la Laisamis, usiku wa kuamkia leo.

Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, amesema mifugo iliyoibwa ni pamoja na ngamia, mbuzi na ng’ombe. Amesema maafisa wa usalama wanaendelea na msako wa mifugo hiyo na wana matumaini ya kuirejesha kwa wenyewe.

Kamishna Kamande amesema huenda tukio hilo ni shambulizi la kulipiza kisasi kufuatia kuibwa kwa ngamia wanane wiki iliyopita katika eneo la Shurr, wadi ya Turbi, ambao walidaiwa kupelekwa katika eneo bunge la Laisamis.

Hata hivyo, amesema idara ya usalama imefanikiwa kuwapata baadhi ya ngamia hao.

Wakati huo huo, Kamishna huyo amezirai jamii zilizoathirika kuwa na subira huku serikali ikiendelea na juhudi za kurejesha mifugo iliyoibwa. Amesisitiza kuwa uchochezi na mashambulizi ya kulipiza kisasi hayasaidii kutatua tatizo, bali huchochea uhasama na kuhatarisha amani katika eneo hilo.

Post Comment