Kanisa kuanzisha majukwaa ya kusikiliza sauti za vijana Afrika Mashariki
Na Silvio Nangori
Baraza la Maaskofu wa kanisa katoliki afrika mashariki na ya kati AMECEA imeazimia kuipa kipaumbele cha kichungaji katika eneo la Afrika Mashariki na kati kwa kuandaa na kutekeleza programu zinazojibu mahitaji ya vijana.
Ili kufanikisha azma hiyo, Kanisa litaanzisha miundo madhubuti ya kuwafundisha na kuwateua makasisi na wahudumu maalumu wa kusimamia huduma kwa vijana.
Kupitia rasimu ya maazimio ya kikao cha mafunzo cha mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA Iliyo wasilishwa na Padri Emmanuel Chimombo ambaye ni mratibu wa taasisi ya kichungaji ya AMECEA, maaskofu na wajumbe walitafakari na kujadili kwa kina mada ya “Safari ya Kisinodi ya AMECEA pamoja na Vijana”
Majadiliano hayo yalilenga namna ya kuwashirikisha vijana katika imani na kukuza maendeleo yao ya jumla kama binadamu.
Baadhi ya maazimio ni kusisitiza umuhimu wa kuandamana na vijana katika kutambua miito yao, kupanga taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika maisha ya jamii na utume wa Kanisa.
Aidha, Kanisa linatumai kuanzisha programu na miundo jumuishi inayowapa nafasi vijana ili kuhakikisha sauti zao zinasikika kupitia majukwaa rasmi katika parokia, majimbo na vyombo vya kitaifa vya Kanisa.
Maaskofu wamekubaliana pia kuimarisha ushirikiano kati ya shule, parokia, jumuiya, familia na taasisi za Kanisa katika huduma kwa vijana pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kiekumene na kidini ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kiuchumi na kiteknolojia zinazowakabili vijana wa sasa.



Post Comment