Washukiwa watatu wakamatwa na vipande sita vya meno ya tembo Laikipia.
Na Nyabande Orwa
Washukiwa watatu wamekamatwa katika kaunti ya Laikipia baada ya kupatikana wakimiliki vipande sita vya meno ya tembo katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na maafisa wa polisi na wale wa huduma ya wanyamapori nchini, KWS.
Polisi wamesema operesheni hiyo ilifanyika jana na kusababisha kupatikana kwa meno hayo ambayo sasa yanahifadhiwa kama ushahidi.
Washukiwa hao wamewekwa rumande wakisubiri kufikishwa mahakamani. Kukamatwa kwao kunajiri wakati mamlaka za usalama na uhifadhi wa wanyamapori zikiendelea kuimarisha vita dhidi ya ujangili na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori, ambayo imeendelea kutishia juhudi za uhifadhi nchini.
Polisi pia wamewahimiza wananchi kutoa taarifa kuhusu shughuli zozote zinazotiliwa shaka ili kusaidia kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.



Post Comment