Highlights

Marsabit yafikia asilimia 72 ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee

Na JB Nateleng

Asilimia 72 ya akina mama katika kaunti ya Marsabit wanawanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya maisha, kama inavyopendekezwa na wataalamu wa afya.

Haya ni kwa mujibu wa mratibu wa lishe katika kaunti ya Marsabit David Buke, ambaye amesema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya ya watoto jimboni.

Akizungumza na shajara, Buke amesema akina mama wengi Marsabit wanaendelea kuzingatia miongozo ya Idara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), inayopendekeza watoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza, na kuendelea kunyonyeshwa sambamba na vyakula vya nyongeza hadi wafikishe umri wa miaka miwili au zaidi.

Buke amesema unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza huimarisha kinga ya mwili, ukuaji na maendeleo ya mtoto, huku pia ukimsaidia mama kupunguza hatari ya kupata baadhi ya magonjwa.

Na huku dunia ikiendelea kuadhimisha wiki ya Kimataifa ya Kunyonyesha kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti 2026, Buke ametoa wito kwa wadau wa sekta ya afya kuendelea kuhamasisha akina mama kuhusu umuhimu wa kuzingatia miongozo ya wataalamu wa afya ili kuboresha afya ya watoto na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya nchini, ni takriban asilimia 60 pekee ya akina mama nchini Kenya wanaowanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya maisha, kiwango kinachowaacha watoto wanne kati ya kila kumi katika hatari ya utapiamlo.

Utapiamlo huo unakadiriwa kusababisha hasara ya kiuchumi ya takriban shilingi bilioni 373 kila mwaka kutokana na athari zake kwa afya na maendeleo ya watoto.

Aidha, ingawa asilimia 89 ya wanawake nchini hujifungua kwa usaidizi wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, ni asilimia 60 pekee ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.

Wataalamu wanasema hali hiyo inawaweka watoto wengi katika hatari ya magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Kauli hii ilitolewa wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa wiki ya kunyonyesha duniani uliofanyika Murang’a.

Post Comment