Highlights

Serikali yaanza uchunguzi wa ugonjwa unaoua ngamia Dukana.

Na Nyabande Orwa

Idara ya mifugo katika eneo bunge la North Horr, kaunti ya Marsabit, imeanzisha uchunguzi kubaini ugonjwa unaosababisha vifo vya ngamia katika eneo hilo.

Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu, mkuu wa Idara ya mifugo North Horr, Dabasso Tuna, amesema serikali ya kaunti ya Marsabit imeanza mchakato wa kukusanya sampuli kutoka kwa ngamia walioathirika na waliosalia hai ili zipelekwe katika maabara ya serikali kwa uchunguzi. Lengo ni kubaini aina ya ugonjwa huo pamoja na chanzo chake ili hatua stahiki zichukuliwe.

Aidha, Dabasso amesema zoezi la kuwachanja mifugo katika maeneo yaliyoathirika limepangwa kuanza katika siku chache zijazo kama sehemu ya juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Wakati huo huo, amewatahadharisha wafugaji dhidi ya kula mizoga ya ngamia waliokufa, akisema kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha afya zao na kusababisha maambukizi ya magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Hatua hizi zinajiri baada ya wakazi wa Dukana mapema wiki hii kuilaumu serikali ya kaunti ya Marsabit kwa kile walichodai ni kuchelewa kuchukua hatua, huku ngamia wao wakiendelea kuangamia kutokana na ugonjwa ambao bado haujatambuliwa. Kwa mujibu wa wafugaji hao, ngamia wanaoathirika hudhoofika, kutoa povu mdomoni na hatimaye kufariki.

Post Comment