Highlights

Wakazi wa Sarima walalamikia fursa za ajira katika mradi wa Lake Turkana Wind Power

Na Nyabande Orwa

Wakazi wa eneo la Sarima, kaunti ndogo ya Loiyangalani, wameitaka kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo ya Lake Turkana Wind Power kuhakikisha fursa za ajira zinatolewa kwa usawa, huku wakiwapa kipaumbele wenyeji wa eneo hilo.

Wakizungumza na Radio Jangwani kwa njia ya simu baada ya kufanya maandamano na kuziba kwa muda barabara kuu ya Sarima–Loiyangalani, wakazi hao wanasema hata kazi za vibarua zinapewa watu kutoka maeneo mengine, huku wakazi wa Sarima wakipata nafasi chache licha ya kampuni hiyo kuendesha shughuli zake katika eneo lao.

Wakazi hao wamedai kuwa walifanya mikutano miwili mwezi uliopita na mmoja wa viongozi wa kampuni anayesimamia masuala ya ajira na kuahidiwa kuwa changamoto hiyo ingepatiwa suluhu ya kudumu.

Hata hivyo, walisema hakuna hatua iliyochukuliwa hadi sasa, jambo lililowalazimu kuandamana ili sauti yao isikike.

Wakazi hao sasa wanazitaka serikali ya kaunti, viongozi wa eneo hilo pamoja na uongozi wa kampuni ya Lake Turkana Wind Power kuingilia kati na kuhakikisha haki inatendeka katika utoaji wa ajira na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii ya Sarima.

Hata hivyo juhudi za kituo hiki kutafuta upande waasimamizi kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo ya Lake Turkana Wind Power hazikufua dafu.

Post Comment