Highlights

Madereva walalamikia ubovu wa barabara ya Marsabit–Loiyangalani.

Na JB Nateleng

Madereva wanaotoa huduma za usafiri wa abiria kati ya Marsabit na Loiyangalani wamelalamikia hali mbaya ya barabara hiyo, wakisema imewalazimu kutumia muda mrefu zaidi kukamilisha safari kutokana na ubovu wake.

Wakizungumza na wanahabari, wakiongozwa na mmoja wa madereva hao, Mohamed Yoro, wamesema barabara hiyo imeharibika kwa kiwango kikubwa, hali inayosababisha uharibifu wa magari na kuongeza gharama.

Yoro amesema sehemu ya barabara kutoka Civicon hadi Loiyangalani ndiyo iliyoathirika zaidi baada ya mvua zilizonyesha, na hadi sasa haijakarabatiwa huku akitoa wito kwa idara husika kuchukua hatua za haraka kuikarabati barabara hiyo ili kurahisisha usafiri na kulinda magari dhidi ya uharibifu.

Yoro ameongeza kuwa madereva wengi sasa wanatumia njia ya Marsabit–Segel–Kargi–Loiyangalani badala ya Marsabit–Hula Hula–Kargi–Loiyangalani kutokana na ubovu wa barabara ya Hula Hula, akidai kuwa haijawahi kufanyiwa ukarabati wa kuridhisha tangu kuanzishwa kwa Serekali ya ugatuzi.

Wakati huo huo, madereva hao wameeleza hofu yao kufuatia utabiri wa hali ya hewa unaoonyesha kuwa Kaunti ya Marsabit inaweza kushuhudia mvua kubwa katika kipindi kijacho wakisema hali hiyo inaweza kuzorotesha zaidi usafiri ikiwa barabara haitakarabatiwa mapema.

Wametoa wito kwa Kamati ya Usimamizi wa Majanga ya Kaunti ya Marsabit kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ifanyiwe ukarabati kabla ya msimu wa mvua kuanza.

Post Comment