Hospitali ya Rufaa ya Marsabit yakana kuwepo kwa mgomo wa wahudumu wa afya
Na Samuel Kosgei
Afisa Msimamizi wa Hospitali Kuu ya Rufaa ya Marsabit, Kusu Abduba, amewataka wakazi wa kaunti hii kuendelea kutafuta huduma za matibabu katika hospitali hiyo licha ya mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya nchini.
Akizungumza na wanahabari, Kusu amesema kuwa tofauti na baadhi ya maeneo mengine nchini, madaktari, wauguzi na maafisa wa kliniki katika Hospitali ya Rufaa ya Marsabit wanaendelea na majukumu yao ya kawaida na kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa huduma chini ya Mpango wa Afya wa Jamii (SHA) zinaendelea kutolewa kwa wote waliosajiliwa. Kwa wale ambao bado hawajajisajili, amesema wanaweza kupata usaidizi kupitia dawati maalum lililoanzishwa hospitalini humo.
Mgomo wa kitaifa wa maafisa wa kliniki ulianza rasmi Julai 20, 2026, baada ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kushindwa kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini yaliyotiwa saini Januari mwaka huu.
Miongoni mwa sababu zilizochochea mgomo huo ni madai kwamba serikali imeshindwa kutimiza ahadi na masharti yaliyoainishwa katika makubaliano hayo. Masuala ya ustawi wa wafanyakazi pamoja na utekelezaji wa mageuzi yaliyokubaliwa katika sekta ya afya bado hayajapatiwa ufumbuzi.



Post Comment