Wahudumu wa matatu wapinga NTSA kudhibiti nauli
Na Abdilaziz Yusuf
Wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma mjini Marsabit wamepinga pendekezo la mswada unaolenga kuipa mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama barabarani (NTSA) mamlaka ya kudhibiti nauli za usafiri wa umma.
Wakizungumza na shajara, wahudumu hao wamesema suluhisho la changamoto ya nauli si kuweka udhibiti wa bei, bali kupunguza gharama za uendeshaji, hususan bei ya mafuta. Wamedai kuwa iwapo mamlaka ya kudhibiti kawi na petroli (EPRA) itapunguza bei ya mafuta, wamiliki wa magari pamoja na wahudumu wataweza kushusha nauli bila kulazimishwa.
Kwa upande wao, madereva wa magari ya uchukuzi wa umma wamesema jukumu la NTSA linapaswa kubaki katika kuhakikisha usalama barabarani na kutekeleza sheria za usafiri, badala ya kuingilia upangaji wa nauli.
Hata hivyo, baadhi ya abiria wameunga mkono pendekezo hilo wakisema linaweza kusaidia kuwalinda wasafiri dhidi ya ongezeko holela la nauli, hasa wakati wa sikukuu na vipindi vya mahitaji makubwa ya usafiri. Wamesema iwapo litatekelezwa kwa haki, hatua hiyo itasaidia kuhakikisha nauli zinabaki za kiwango kinachomudu wananchi.



Post Comment