Highlights

Serikali yahimiza vijana wa Marsabit kujifunza ujuzi wa kujitegemea

Na Nyabande Orwa

Mkurugenzi wa masuala ya vijana kutoka serikali Kuu, Joseph Maina, amewahimiza vijana wa kaunti ya Marsabit kujitokeza na kujifunza ujuzi wa kazi mbalimbali ili kujitegemea kiuchumi na kupunguza ukosefu wa ajira.

Akizungumza na Radio Jangwani wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya vijana waliochaguliwa kushiriki katika mpango wa serikali wa ukuzaji wa ujuzi, Maina amesema washiriki wataanza kwa mafunzo ya siku 20 ya kuwaandaa kabla ya kupelekwa kwenye mafunzo ya vitendo chini ya mafundi waliobobea katika fani mbalimbali ikiwemo useremala, ujenzi, ufundi wa magari na pikipiki.

Vijana 1,420 kutoka Marsabit watanufaika na mpango huo. Alieleza kuwa tofauti na mpango wa NYOTA uliowapatia baadhi ya vijana ruzuku ya kuanzisha biashara, mpango huu unalenga kuwapatia ujuzi wa kudumu utakaowawezesha kujiajiri au kupata ajira.

Kitaifa, mpango wa NYOTA unalenga kuwafikia vijana 820,000 wasio na ajira, huku 90,000 wakitarajiwa kupata mafunzo ya ujuzi na mafunzo ya vitendo kupitia mfumo wa uanagenzi katika kaunti zote 47.
Kwa upande wao, vijana waliohudhuria hafla hiyo wameishukuru serikali kwa kuanzisha mpango huo wakisema utasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Baadhi yao hata hivyo waliitaka serikali kuharakisha utoaji wa nafasi za ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi ili kuhakikisha ujuzi unaopatikana unaendana na fursa za ajira nchini.

Post Comment