Highlights

Wafugaji Dukana walilia serikali kusaidia kukabili ugonjwa wa mifugo

Wafugaji katika eneo la Dukana, kaunti ya Marsabit, wameitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuingilia kati haraka kukabiliana na ugonjwa unaodaiwa kuendelea kuangamiza mifugo, hususan ngamia.

Wafugaji hao wanasema wamekuwa wakipoteza mifugo kwa kiwango kikubwa kutokana na ugonjwa ambao chanzo chake bado hakijabainika, hali inayotishia maisha na uchumi wa jamii inayotegemea ufugaji.

Akizungumza na kituo hiki, mzee Kizito Konchoro amesema wafugaji hawajapata huduma za chanjo za mifugo kwa muda mrefu.

Konchoro anasema dalili zinazojitokeza kwa ngamia wanaougua ni pamoja na kushindwa kukojoa, kuvimba mwili, kutoa makamasi na machozi mengi kabla ya kufa baada ya muda mfupi.

Naye mfugaji Guyo Hukha ameiomba serikali na washikadau wa sekta ya mifugo kuharakisha uchunguzi wa ugonjwa huo na kutoa chanjo pamoja na huduma za matibabu ili kuokoa mifugo waliosalia.

Hata hivyo juhudi za kituo hiki kutafuta  upande wa wizara ya mifugo kaunti ya marsabit hazikufua dafu.

Post Comment