Rais Ruto atia saini sheria ya fedha 2026, akisema hakuna ushuru mpya
Na Nyabande Orwa
Rais William Ruto amesema kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2026 haijaweka ushuru mpya kwenye huduma za M-Pesa, mitumba, ardhi, maji, simu za mkononi, muda wa maongezi wala data. Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi wakati wa kutia saini mswada huo kuwa sheria, Ruto alisema taarifa zilizokuwa zikienea kuhusu ushuru huo zilikuwa za kupotosha na hazikuwa za kweli.
Rais alisema sheria hiyo inalenga kuboresha usimamizi wa kodi kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuhakikisha watu binafsi pamoja na biashara zinalipa kodi zinazostahili kisheria. Aliongeza kuwa mswada huo ulipitishwa baada ya ushirikishwaji mkubwa wa umma uliowashirikisha maelfu ya Wakenya na mashirika mbalimbali.
Aidha, sheria hiyo imeweka motisha kwa uwekezaji katika teknolojia ya nishati safi ikiwemo pikipiki na mabasi ya umeme, huku ushuru wa sukari inayoagizwa kutoka nje ukiongezwa ili kulinda viwanda vya sukari vya nchini. Ruto pia alitangaza msamaha wa miezi sita wa riba na adhabu kwa madeni ya kodi yaliyochelewa kulipwa.



Post Comment