Highlights

Sehemu kubwa ya Marsabit kutarajiwa kusalia kavu wiki hii

Sehemu kubwa ya Kaunti ya Marsabit zinatarajiwa kuendelea kushuhudia hali ya ukavu katika kipindi cha kuanzia leo Juni 23 hadi 29, mwaka huu, kulingana na utabiri wa hali ya hewa.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa manyunyu zozote zitakazoshuhudiwa zinatarajiwa katika maeneo machache, hasa kando ya mpaka wa Ethiopia, eneo la Mlima Marsabit na nyanda za juu za Sololo.

Wakati uo huo, maeneo ya nyanda za juu yanatarajiwa kushuhudia hali ya baridi na mawingu nyakati za asubuhi, huku maeneo ya tambarare na bonde la Ziwa Turkana yakikabiliwa na joto kali pamoja na upepo mkali.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wamehimizwa kutumia kwa uangalifu vyanzo vya maji vilivyopo kwani ukavu unatarajiwa kuendelea katika sehemu kubwa ya kaunti.

Wafugaji pia wametakiwa kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa malisho na maji kwa mifugo yao, hasa katika maeneo ya chini yanayotegemea ufugaji.

Aidha, wavuvi na watumiaji wa Ziwa Turkana wameonywa kuwa waangalifu kutokana na matarajio ya upepo mkali na mawimbi makubwa yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Madereva nao wamehimizwa kuwa waangalifu barabarani kutokana na uwezekano wa kupungua kwa mwonekano kunakoweza kusababishwa na vumbi katika maeneo ya tambarare na ukungu wa asubuhi katika maeneo ya nyanda za juu.

Maeneo kadhaa nchini yanatarajiwa kushuhudia hali ya hewa ya baridi na mawingu ya hapa na pale katika kipindi cha wiki hii, kulingana na utabiri wa hivi punde wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Kenya.

Katika utabiri wake wa kipindi cha Juni 23 hadi Juni 29, 2026, idara hiyo imesema hali hiyo ya hewa itashuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Nyanda za Chini za Kusini Mashariki, Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Idara hiyo pia imetabiri kuwa mvua zitanyesha katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ufa, Ukanda wa Pwani na sehemu za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Post Comment