Wanafunzi wa dini ya Kiislamu katika shule za umma Marsabit waruhusiwa kuvalia vazi la hijabu
Na Caroline Waforo
Baraza la Viongozi wa Kidini (Interfaith Council) tawi la Marsabit, limetia saini mkataba wa maelewano unaowaruhusu wanafunzi wa dini ya Kiislamu katika shule za umma kuvalia vazi la hijabu.
Mkataba huo umetiwa saini leo Jumanne na viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu katika hafla iliyofanyika katika hoteli moja mjini Marsabit.
Hafla hiyo imeandaliwa na Baraza la Madhehebu Mbalimbali nchini (Inter-Religious Council of Kenya – IRCK), kwa ushirikiano na mashirika ya Christian Aid na Islamic Relief Kenya.
Kupitia taarifa ya pamoja, viongozi hao wamezitaka shule zote za umma katika kaunti ya Marsabit kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo ili kuimarisha uhuru wa kuabudu, mshikamano na amani katika taasisi za elimu.
Mwenyekiti wa Baraza la Viongozi wa Kidini tawi la Marsabit ambaye pia ni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Marsabit, Mhashamu Peter Kihara, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha maelewano na kuheshimu haki za wanafunzi wa dini zote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madhehebu Mbalimbali nchini, Sheikh Abdullahi Salat, amepongeza viongozi hao wa dini kwa kufikia mwafaka huo.
Amesema kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kuhusu uvaaji wa hijabu katika shule za umma itaondolewa rasmi kufuatia makubaliano hayo.
Naye Naibu Kamishna wa Marsabit Central Stanley Kamande, amesema mwafaka huo umeondoa mzozo uliokuwa unatishia kuathiri sekta ya elimu katika kaunti ya Marsabit.
Serikali ya kaunti ya Marsabit pia imepongeza pakubwa mwafaka huo ambao umehitimisha mvutano wa muda mrefu kuhusu iwapo wanafunzi wa Kiislamu wanapaswa kuruhusiwa kuvalia hijabu katika shule za umma.
Miongoni mwa shule zilizokuwa zimehusishwa na mjadala huo ni Shule ya Msingi ya St. Teresa iliyoko mjini Marsabit na Shule ya Msingi ya Consolata iliyopo Maikona eneo bunge la North Horr



Post Comment