Jamaa afikishwa kortini kwa tuhuma za kuchoma pikipiki Marsabit
Na Mwandishi wetu
Mwanamume mmoja amefikishwa katika mahakama ya Marsabit akikabiliwa na shtaka la kuharibu mali kwa kuteketeza pikipiki, tukio linalodaiwa kutokea tarehe 25 Juni mwaka jana.
Mbele ya hakimu mkuu mkazi wa mahakama ya Marsabit, Christine Wekesa, upande wa mashtaka ulidai kuwa mshukiwa, Mustafa Said Jillo, aliteketeza pikipiki inayomilikiwa na mlalamishi, Suleiman Hido Shano.
Jillo alikamatwa tarehe 17 Julai mwaka huu na kuzuiliwa na polisi kabla ya kufikishwa mahakamani leo Jumatatu.
Hata hivyo, hakimu Wekesa ameamuru mshukiwa apelekwe hospitalini kwa matibabu baada ya kulalamika kuwa alikuwa hajisikii vizuri. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 27 Julai kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi la kuachiliwa kwa mshukiwa kwa dhamana.



Post Comment