KUPPET Marsabit yasema walimu wanaojihusisha kimapenzi na Wanafunzi kuchukuliwa hatua za kisheria
Na JB Nateleng
Katibu Mkuu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri (KUPPET) tawi la Marsabit, Sarr Galgallo, amesema mwalimu yeyote atakayepatikana akiwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi au kumdhalilisha mwalimu mwenzake kingono anapaswa kuwajibishwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Sarr amesema walimu wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kukuza maadili mema yanayojenga jamii yenye misingi imara akisisitiza kuwa KUPPET haitamtetea wala kumlinda mwalimu yeyote atakayebainika kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi.
Aidha, amesema jukumu la mwalimu ni kufundisha na kulea wanafunzi kimaadili, si kuwatumia kingono, akibainisha kuwa uhusiano wa kimapenzi kati ya mwalimu na mwanafunzi ni kosa la kisheria na la kinidhamu.
Wakati huo huo, Sarr ameitaka serikali kuongeza marupurupu ya walimu wanaosimamia shughuli za michezo, akisema kiwango cha sasa hakitoshi kuwapa motisha wa kutekeleza majukumu hayo.
Kwa upande wa huduma za afya, Sarr amewahimiza walimu kujiandikisha na kuchangia bima ya SHA, akisema mpango huo una manufaa makubwa kwa afya zao akiongeza kuwa mwalimu aliyesajiliwa na kulipia SHA hapaswi kutozwa gharama za matibabu katika hospitali zinazotoa huduma chini ya mpango huo.



Post Comment