Highlights

Mawakili Marsabit wasusia mahakama kulalamikia ufisadi.

Na Nyabande Orwa

Mawakili katika kaunti ya Marsabit leo wamesusia kufika mahakamani kuwatetea wateja wao wakilalamikia kile wanachodai ni changamoto katika mfumo wa utoaji wa haki, hususan madai ya ufisadi ndani ya idara ya mahakama.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa chama cha mawakili nchini (LSK) tawi la Marsabit, John Behailu, madai ya ufisadi katika mahakama yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu, lakini bado tume ya huduma za mahakama (JSC) haijachukua hatua zinazostahili kuyashughulikia.

Behailu ameongeza kuwa wananchi hutumia fedha nyingi kufuatilia kesi zao, lakini baadhi yao hukosa haki kutokana na kile alichodai kuwa ni ushawishi usiofaa katika utoaji wa maamuzi ya mahakama. Amesema hali hiyo pia imechangia kesi nyingi kuchukua muda mrefu kabla ya kuamuliwa.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuripoti visa vyovyote vya rushwa au ukiukaji wa maadili vinavyohusisha maafisa wa mahakama kupitia ofisi ya LSK mjini Marsabit ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Behailu pia amewataka wakazi wa kaunti hii kuwa waangalifu dhidi ya mawakili bandia wanaojihusisha na utoaji wa huduma za kisheria bila idhini.

Wakili huyo amesema kuwa kuna baadhi ya watu katika kaunti ya Marsabit wanaojitambulisha kama mawakili ilhali hawana vyeti wala leseni zinazowaruhusu kutoa huduma za kisheria.

Aidha, amesema kuwa kila kampuni ya uwakili (law firm) inapaswa kuwa na angalau wakili aliyesajiliwa rasmi na Chama cha Mawakili Nchini pamoja na cheti halali cha kufanya kazi, huku wafanyakazi wengine wa ofisi hiyo wakiwa wameidhinishwa kwa mujibu wa sheria.

Behailu amewaonya wananchi kuwa kutumia huduma za mawakili wasioidhinishwa kunaweza kusababisha hasara kubwa, ikiwemo kesi zao kutupiliwa mbali mahakamani kutokana na kutowakilishwa kisheria ipasavyo.

Post Comment