Idara ya trafiki Marsabit yaonya waendesha bodaboda dhidi ya kutumiwa kisiasa.
Na Nyabande Orwa
Idara ya trafiki katika kaunti ya Marsabit leo imekutana na wahudumu wa sekta ya bodaboda katika juhudi za kuimarisha usalama barabarani, kukabiliana na vitendo vya kihuni na kuhimiza uzingatiaji wa sheria za trafiki.
Katika kikao hicho, maafisa wa idara hiyo wamewataka waendesha bodaboda kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuchochea au kuzua vurugu, wakisema hatua hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na kuleta hofu katika jamii.
Aidha, wamewahimiza wahudumu hao kuzingatia maadili ya kazi kwa kuvaa mavazi yanayofaa wanapokuwa kazini, kutumia vifaa vya kujikinga kama vile kofia ngumu, na kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya wanapoendesha pikipiki.
Wakati huo huo, Idara ya Trafiki imewataka waendesha bodaboda kutoa taarifa za ajali mara zinapotokea ili kuwezesha uchunguzi na kubaini hatua za kuzuia matukio kama hayo siku zijazo.
Pia imewahimiza watumiaji wote wa barabara kuheshimiana na kufuata sheria za usalama barabarani. Vile vile , waendesha bodaboda wamehimizwa kujiunga na kuunda vikundi vya ushirika ili kuimarisha uongozi, uwajibikaji na ustawi wa sekta hiyo.



Post Comment