Washikadau wa NRM wakutana Marsabit kuimarisha usimamizi wa Mali asili.
Na JB Nateleng
Washikadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali ya kitaifa na serikali ya Kaunti ya Marsabit wamekutana leo katika kongamano lililofadhiliwa na shirika la Centre for Research and Development in Drylands (CRDD) kujadili masuala ya Usimamizi wa Mali asili (NRM).
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo, Afisa Mkuu wa Idara ya Maliasili na Wanyamapori katika Kaunti ya Marsabit na mwenyekiti wa NRM, Pauline Marleni, amesema kongamano hilo limewapa washikadau fursa ya kubadilishana taarifa kuhusu shughuli wanazotekeleza na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa maliasili.
Marleni ameongeza kuwa serikali ya kaunti inajiandaa kuwasilisha miswada itakayosaidia kusimamia sekta ya maliasili, akisema maoni yaliyotolewa katika mkutano huo yatachangia kuandaliwa kwa sheria na kanuni zitakazoimarisha usimamizi wa rasilimali hizo.
Kwa upande wake, mratibu wa programu na utafiti katika shirika la Centre for Research and Development in Drylands (CRDD), Abdinasir Elmi, amesema kongamano hilo hufanyika kila robo mwaka na huwakutanisha washikadau mbalimbali ili kujadili changamoto zinazojitokeza na kutafuta suluhisho la pamoja.
Abdinasir amesema CRDD inapanga kuanzisha programu ya utafiti itakayowasaidia wafugaji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwapa taarifa na mikakati ya kupanga shughuli zao kwa ufanisi, hatua ambayo inatarajiwa kuboresha maisha ya jamii za wafugaji katika kaunti hiyo.



Post Comment