Highlights

Wakazi wa Kamboe walalamikia ukosefu wa mtandao wa mawasiliano

Na JB Nateleng

Wakazi wa Kamboe, wadi ya Karare katika kaunti ya Marsabit, wameitaka serikali kushughulikia tatizo la ukosefu wa mtandao wa mawasiliano, wakisema linaathiri usalama, huduma za afya na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Akizungumza na idhaa hii, nesi wa zahanati ya Kamboe, John Lenareyo, amesema ukosefu wa mtandao umetatiza utoaji wa huduma za afya, hususan usajili wa wagonjwa katika mpango wa afya ya Jamii (SHA) akisema mtandao duni unachelewesha ukusanyaji wa taarifa za kibiometriki zinazohitajika wakati wa usajili wa wagonjwa.

Anasema kutokana na tatizo hilo, wahudumu wa afya hulazimika kutembea takribani kilomita mbili pamoja na wagonjwa ili kupata mtandao na kukamilisha usajili wa SHA kabla ya kurejea zahanatini kwa matibabu.

Mbali na sekta ya afya, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na mzee Suproi Letapo, mzee Ltereyon Ejet na Eunice Letole wamesema ukosefu wa mtandao umeathiri biashara na wakati mwingine wafanyibiashara  hushindwa kuwasiliana na wasambazaji kuagiza bidhaa jambo ambalo linawalazimu kusafiri hadi Log Logo ili kutuma au kutoa fedha kupitia huduma za simu.

Wakazi hao wameomba serikali kuharakisha ujenzi au uboreshaji wa mnara wa mawasiliano kwenye eneo hilo kwa manufaa ya maisha ya kawaida.

Post Comment