Walimu wakuu Marsabit watakiwa kuzingatia mwongozo wa usalama shuleni
Walimu wakuu wa taasisi za elimu kaunti ya Marsabit hususan shule za upili za mabweni, wametakiwa kuzingatia kikamilifu mwongozo wa usalama shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma na kuishi katika mazingira salama.
Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake leo Jumatatu, Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Marsabit Williams Kamuguna, amesema kuwa wadau wa elimu jimboni wamekuwa wakifanya ziara katika shule mbalimbali ili kutathmini viwango vya usalama na hali ya mazingira shuleni.
Hii ni kutokana na wimbi la migomo, visa vya moto na vurugu za wanafunzi linaloendelea kuzua hofu kubwa katika sekta ya elimu baada ya shule kadhaa za upili kufungwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamuguna amewahimiza walimu wakuu kuhakikisha vigezo vyote vimezingatiwa ipasavyo, ikiwemo kuwapa wanafunzi chakula bora na cha kutosha, hatua ambayo amesema itasaidia kudumisha nidhamu na kuzuia vurugu shuleni.
Aidha amesema kuwa shule nyingi katika kaunti ya Marsabit zinaendelea kushuhudia utulivu, ikiwemo Shule ya Upili ya Gadamoji iliyoko kaunti ndogo ya Marsabit Central, ambapo wiki iliyopita baadhi ya wanafunzi walidaiwa kuondoka shuleni wakilalamikia uhaba wa maji pamoja na hali ya chakula walichokuwa wakipewa.
Wakati huo huo, Kamuguna ametoa onyo kali kwa wazazi wanaowanyima watoto haki ya kupata elimu kwa kuwaoza kwa mapema akisema kuwa mamlaka husika hazitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayepatikana akihusika na vitendo hivyo.



Post Comment