Highlights

Wadau wa elimu Marsabit wawataka wanafunzi Kukumbatia ubunifu na akili unde kutatua changamoto za Jamii

Na JB Nateleng

Mkurugenzi wa Elimu kaunti ya Marsabit, William Kamugunah, amewataka wanafunzi kuendeleza ubunifu na uvumbuzi ili wawe sehemu ya kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Akizungumza katika Maonyesho ya Sayansi ya kaunti ya Marsabit yaliyofadhiliwa na Datatec kupitia shirika la Concern Worldwide, Kamugunah amesema ni muhimu kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa ubunifu tangu wakiwa wadogo ili waweze kubuni suluhisho endelevu kwa matatizo yanayoikabili jamii.

Kamugunah pia amewahimiza waandaaji wa maonyesho hayo kuruhusu shule ambazo hazijashiriki kufika na kujionea miradi mbalimbali ili kuwapa motisha ya kujifunza na kuelewa matumizi ya teknolojia ya Akili Unde.

Kwa upande wake, Afisa msimamizi wa rasilimali ya watu wa TSC kaunti ya Marsabit, Dae Kane, aliyemwakilisha mkurugenzi wa TSC tawi la Marsabit, amewataka walimu kuwafundisha wanafunzi matumizi sahihi ya Akili Unde katika maisha ya kila siku akisisitiza umuhimu wa kuwaelekeza kuhusu fursa pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo.

Post Comment