Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba apongeza mchango wa AMECEA katika kuimarisha utume wa kanisa.
Na Silvio Nangori
Mwenyekiti wa baraza la maaskofu katoliki Kenya (KCCB), Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba, amesema jumuiya ya mabaraza ya maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) imeendelea kuwa mwaminifu kwa dhamira yake ya kujibu mahitaji na hali halisi ya maisha ya watu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA unaofanyika katika chuo kikuu cha kikatoliki cha Afrika MASHARIKI (CUEA) jijini Nairobi, Askofu Mkuu Muhatia amesema vipaumbele vya kichungaji vya AMECEA vimekuwa vikiongozwa na matumaini, changamoto na matarajio ya waamini na jamii zinazohudumiwa na Kanisa.
Amesema kuwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki kilikuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 17 wa AMECEA miaka 15 iliyopita, wakati Kanisa lilipoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa AMECEA.
Akizungumzia uhusiano wa karibu kati ya AMECEA na CUEA, Askofu Mkuu Muhatia amesema hata kufanana kwa vifupisho vya majina yao kunaashiria ushirikiano wa karibu kati ya Baraza la Maaskofu wa ukanda huu na chuo hicho katika kuendeleza utume wa Kanisa.
Aidha, ameelezea historia ya AMECEA kupitia kaulimbiu za mikutano yake ya awali, akibainisha kuwa Kanisa limeendelea kushughulikia masuala muhimu ya kijamii, kichungaji na kiroho yanayoikabili Afrika Mashariki.
Amesema Mkutano Mkuu wa 14 uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania mwaka 2002 ulijikita katika kuimarisha uinjilishaji katika milenia mpya, huku Mkutano Mkuu wa 15 uliofanyika Mukono, Uganda mwaka 2005 ukijadili changamoto ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI katika ukanda huo.
Vilevile, ameema Mkutano Mkuu wa 16 uliofanyika Lusaka, Zambia mwaka 2008 ulijadili kaulimbiu ya Maridhiano kupitia Haki na Amani, ambayo amesema bado ina umuhimu mkubwa hadi leo, hasa nchini Kenya.



Post Comment