Wananchi Wapongezwa kwa Kudumisha Amani Wakati wa Uchaguzi wa Ol-Kalau
Na Abdiaziz Yusuf
Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Mohamed Hassan amesema licha ya wanasiasa kutumia rasilimali nyingi kuwashawishi wapiga kura, uamuzi wa mwisho hubaki mikononi mwa wananchi.
Akizungumza na Shajara siku moja baada ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol-Kalau kukamilika, Mohamed amesema wapiga kura wana uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu mgombea wanayemtaka, bila kujali kiasi cha fedha kinachotumika katika kampeni.
Mohamed pia amewapongeza wananchi wa Ol-Kalau kwa kudumisha amani wakati wa uchaguzi huo, akisema walijitokeza kwa utulivu kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura. Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na vyombo vya usalama ulichangia kufanikisha uchaguzi wa amani, huku akihimiza jamii kuendelea kuishi kwa umoja licha ya tofauti za kisiasa.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Vijana katika Kaunti ya Marsabit, Abdilaziz Boru, amewataka vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuchochea machafuko au kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.



Post Comment