Kamishna Stanley Kamande awaonya wakazi wa Dabel dhidi ya uchimbaji haramu wa dhahabu.
Na Nyabande Orwa
Kamishna wa kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, amewaonya wakazi wa eneo la Dabel dhidi ya kujihusisha na uchimbaji haramu wa madini, akisisitiza kuwa eneo hilo bado liko chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya usalama.
Akizungumza na kituo hiki, Kamande amesema kuwa maafisa wa polisi kwa ushirikiano na idara nyingine za usalama wanaendelea kulinda eneo hilo ili kuzuia kurejea kwa mivutano iliyoshuhudiwa awali na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zitakapofunguliwa zinafanyika kwa njia salama na iliyo katika utaratibu unaokubalika.
Kamande amesema serikali, kupitia wizara ya madini na uchumi samawati, tayari imeanzisha mchakato wa kufungua tena shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.
Kauli hiyo inajiri siku chache baada ya baadhi ya wakazi wa Dabel kulalamikia kile walichodai kuwa ni dhuluma na matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa baadhi ya maafisa wa usalama.
Hata hivyo, kamishna Kamande amepuuzilia mbali madai hayo, akisema operesheni za usalama zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na zinalenga kulinda usalama wa wananchi pamoja na rasilimali za taifa.



Post Comment