Gavana Mohamud Ali ataka ahadi za rais zitekelezwe.
Na Nyabande Orwa
Gavana wa Marsabit, Mohamud Ali, ameihimiza serikali ya Rais William Samoei Ruto kutekeleza kwa haraka ahadi za maendeleo ilizotoa kwa wakazi wa kaunti hii wakati wa mkutano uliofanyika Ikulu, Nairobi, wiki chache zilizopita.
Akizungumza katika harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya makundi ya wanawake wa eneo bunge la Laisamis iliyofanyika katika shule ya msingi ya Loglogo, gavana Mohamud amesema utekelezaji wa miradi hiyo utachangia kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kuboresha huduma kwa wakazi wa Marsabit.
Katika hafla hiyo, waziri wa ulinzi Soipan Tuya, aliyekuwa mgeni wa heshima, amesema makundi ya wanawake yana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na kwamba yanafaa kuendelea kupewa uwezo wa kiuchumi kupitia mipango kama hiyo.
Harambee hiyo iliandaliwa kwa ajili ya makundi zaidi ya 300 ya wanawake yaliyoungana chini ya mwavuli wa Laisamis Women Caucus, kwa lengo la kuimarisha shughuli zao za kujikimu na maendeleo ya kijamii.
Wakati uo huo, waziri, Soipan amesema serikali kupitia Wizara ya ulinzi imeimarisha juhudi za kuimarisha usalama na kukabiliana na wizi wa mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Tuya amesema hatua zilizochukuliwa zimechangia kuimarika kwa hali ya usalama katika maeneo mengi yaliyokuwa yakikumbwa na visa vya wizi wa mifugo na mashambulizi ya mara kwa mara.
Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo yakiwemo kaunti za Samburu, Turkana na Marsabit pamoja na maeneo mengine yanayokumbwa na utovu wa usalama.



Post Comment