Highlights

Mratibu wa lishe Marsabit aonya dhidi ya uuzaji wa vibadala vya maziwa ya mama.

Na JB Nateleng

Kuuza, kutangaza au kutoa mchango wa vibadala vya maziwa ya mama bila kuzingatia masharti yaliyowekwa ni kinyume cha sheria, na yeyote atakayepatikana akikiuka sheria hiyo anaweza kukamatwa na kushtakiwa.

Haya ni kwa mujibu wa mratibu wa lishe katika Kaunti ya Marsabit, David Buke, ambaye amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na wizara ya afya nchini vinapendekeza watoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya maisha, kwa kuwa maziwa hayo hutoa kingamwili muhimu na lishe bora kwa ukuaji wa mtoto.

Hata hivyo, amesema maziwa vinginevyo vinaweza kutumika katika hali maalumu za kiafya za mama, lakini vinapaswa kupendekezwa na mtaalamu wa afya ili kuhakikisha maslahi ya mtoto yanalindwa.

Buke amewakosoa baadhi ya akina mama wanaoacha kuwanyonyesha watoto wao kwa muda unaopendekezwa kwa sababu za urembo wa mwili akisema hatua hiyo inaweza kuathiri afya na ukuaji wa mtoto.

Kulingana na Buke, ukosefu wa fedha umekuwa changamoto kubwa katika juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji akiwataka wahisani na wadau mbalimbali kushirikiana na serikali kufadhili kampeni za kuelimisha wananchi kuhusu manufaa ya maziwa ya mama.

Mnamo Septemba 2012, Bunge la Kenya lilipitisha Sheria ya kudhibiti uuzaji wa vibadala vya maziwa ya mama. Sheria hiyo ilidhihirisha dhamira ya Kenya ya kutekeleza Kanuni za Kimataifa za WHO kuhusu masoko ya vibadala vya maziwa ya mama, ambazo zinalenga kulinda, kuhamasisha na kuunga mkono unyonyeshaji kama njia bora ya kuhakikisha watoto wachanga wanapata lishe inayofaa kwa ukuaji na maendeleo yao.

Post Comment