Maaskofu washabikia kauli mbiu ya Kongamano la 21 la AMECEA 2026
Na Silvio Nangori
Maaskofu wameishabikia kauli mbiu ya kongamano la 21 la AMECEA inayolenga kujenga madaraja ya ushirika, matumaini, haki na utawala bora pamoja na vijana wakisema imegusa kwa kina dhamira ya Kanisa ya kuandamana na kizazi cha sasa katika utume wa uinjilishaji.
Akizungumza katika mahojiano pembezoni mwa mkutano huu unaoendelea jijini Nairobi Askofu Severini Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rurenge, Ngara, kutoka nchini Tanzania amesema mada ya mwaka huu imeibua tafakari ya kina kuhusu nafasi ya vijana ndani ya Kanisa na umuhimu wa kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wake.
Askofu Niwemugizi anasema kwa takribani miaka 29 ya huduma kama askoAskofu ambaye amehudhuria mikutano mingi ya AMECEA, mkutano wa mwaka huu umejitokeza kwa upekee kutokana na uzito wa mada yake na namna ilivyovuta ushiriki na tafakari ya kina miongoni mwa Maaskofu.
Kwa mujibu wake, mkutano huu unatoa fursa ya kujifunza kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kutafakari mustakabali wa Kanisa katika majimbo mbalimbali, hususan kuhusu namna bora ya kuandamana na vijana na kuwajengea mazingira ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kanisa.
Askofu Niwemugizi anasema ujumbe uliotolewa na vijana mapema leo umeonyesha wazi kuwa wengi wao wana ari, vipaji na utayari wa kulitumikia Kanisa, lakini kwa upande mwingine wanahisi kuachwa pembeni na kutopatiwa mwongozo na usindikizaji wa kutosha.
Na kwamba kutokana na hali hiyo Maaskofu wa nchi wanachama wa AMECEA watatumia mkutano huu kujitathmini kwa pamoja ili kubaini maeneo yaliyohitaji kuboreshwa na kuweka mikakati itakayowezesha Kanisa kuimarisha ushiriki wa vijana katika ngazi zote za maisha na utume wake.
Aidha, ameonesha matumaini kuwa maazimio na mafunzo yatakayopatikana katika mkutano huu yatakuwa chachu ya kuimarisha huduma kwa vijana, si tu nchini Tanzania bali katika Kanisa lote katika ukanda Wa AMECEA ili kujenga kizazi chenye matumaini, kinachoshiriki kikamilifu katika uinjilishaji na maendeleo ya jamii.



Post Comment