ASKOFU Odonya kuhusu matumizi ya Kidijitali ili kuwasilisha katekesi Na mafundisho ya kanisa Kwa vijana ”DIGITAL CATECHESIS ‘
Na Silvio Nangori
Mwenyekiti wa Tume ya Vijana katika Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) Askofu Henry Juma Odonya amesema Kongamano la 21 la AMECEA limekuwa jukwaa muhimu la kutafakari namna bora ya kuandamana na vijana katika mazingira yanayobadilika kwa kasi huku likitoa nafasi ya kujadili masuala yanayogusa maisha yao ya kiroho, kijamii na kiuongozi.
Askofu Odonya ameeleza kuwa Kanisa lina wajibu wa kuwasikiliza vijana, kuwashirikisha katika maamuzi na kuwapa nafasi ya kuchangia maendeleo ya Kanisa kuanzia ngazi ya parokia akibainisha kuwa ushiriki wa vijana katika halmashauri za parokia ni hatua muhimu ya kuwajengea uwajibikaji na kuwafanya wajione kuwa sehemu ya utume wa Kanisa.
Askofu vile vile amesisitiza kuwa mjadala wa kongamano hiI unajengwa katika misingi ya Sinodi ya kutembea kwa pamoja, inayohimiza ushirikiano, matumaini, haki na uongozi bora. Kwa mujibu wake, uongozi wenye maadili ndani ya Kanisa na katika jamii ni msingi wa kuwajengea vijana mazingira salama ya kukua na kutimiza ndoto zao.
Askofu Odonya pia ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa zinazolikabili Kanisa ni namna ya kuwafikia vijana katika ulimwengu wa kidijitali bila kupoteza msingi wa Injili japo kama tume ya vijana Katika Baraza la Maaskofu KCCB wameanza kuweka mikakati ya kuimarisha matumizi ya Kidijitali ili kuwasilisha katekesi Na mafundisho ya kanisa Kwa vijana katika mfumo Wa Digital Catechesis kama njia ya kisasa ya kufundisha na kueneza imani kwa vijana, akisisitiza kuwa mbinu hizi zinaweza kubadilika kulingana na wakati, lakini ujumbe wa Yesu Kristo unabaki kuwa ule ule.
Askofu ame,eleza kuwa katekesi ndiyo msingi wa kuijenga imani imara akionya kuwa vijana wasipopewa malezi ya kutosha ya kiimani huwa rahisi kuyumbishwa na changamoto na misukumo ya ulimwengu wa leo akisisitiza kuwa jukumu hilo haliishii kanisani pekee, bali linahitaji ushirikiano wa familia, shule na jamii nzima ili vijana waweze kukua katika maadili na misingi thabiti ya Kikristo.
Kwa upande wa familia, Askofu Odonya amewahiza wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao kuhusu masuala ya imani na kuwalea katika mazingira yanayowajenga kiroho akisema familia ndiyo shule ya kwanza ya imani, hivyo mchango wake ni muhimu katika kuwasaidia vijana kusimama imara mbele ya changamoto mbalimbali.
Askofu hata hivyo ameleza matumaini yake kuwa maazimio yatakayofikiwa katika Kongamano hili la 21 la AMECEA yatawekwa katika vitendo katika majimbo na parokia mbalimbali, ili kuimarisha huduma kwa vijana na kuwajengea mustakabali wenye matumaini, imani na ushiriki mkubwa zaidi katika maisha ya Kanisa na jamii



Post Comment