Rais Ruto ampongeza Museveni kwa kuchaguliwa tena, huku akisifu ukomavu wa demokrasia nchini Uganda
Na Samuel Kosgei
Rais William Ruto amemtumia ujumbe wa pongezi Rais mteule wa Uganda Yoweri Museveni kufuatia kutangazwa kwa kuchaguliwa kwake tena katika uchaguzi uliofanyika Januari 17, 2026.
Katika ujumbe wake wa pongezi, Rais Ruto amesema matokeo hayo yanaakisi imani ambayo wananchi wa Jamhuri ya Uganda wanayo kwa uongozi wake binafsi pamoja na imani waliyo nayo kwa chama cha NRM.
Rais Ruto pia amesifu uchaguzi huo akisema ulikuwa wa amani, na kuwapongeza wananchi wa Uganda kwa kuendelea kuimarisha taasisi za kidemokrasia.
Aidha, amesisitiza uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda, huku akithibitisha tena dhamira ya Kenya kuendeleza ushirikiano wa kikanda.
Kuchaguliwa tena kwa Rais Museveni kunaongeza muda wake wa uongozi uliodumu kwa miongo kadhaa, na kunavutia hisia za kikanda wakati Afrika Mashariki ikiendelea kukabiliana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
Museveni mwenye umri wa miaka 81 alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Uganda uliofanyika Januari 15, 2026, na hivyo kuanza muhula wake wa saba madarakani.



Post Comment