Highlights

Watoto wa Afrika wataka hatua zaidi kukabiliana na changamoto zao.

Na Nyabande Orwa

Serikali kuu kwa ushirikiano na washikadau mbalimbali inaweka mikakati ya kuboresha maisha ya watoto kwa kuangazia masuala ya maji, usafi wa mazingira na usafi wa kibinafsi alaarufu kama SHA.

Haya yamesemwa na afisa wa baraza la kitaifa la huduma za watoto, Joseph Iha Wanje, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika Shule ya SKM mjini Marsabit kwa niaba ya serikali kuu.

Iha Wanje amesema kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana, watoto wengi wa Afrika bado wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hususan ukosefu wa maji safi na salama.

Amesema kaunti ya Marsabit ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame na uhaba wa maji, akitoa wito kwa washikadau wote kushirikiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kukua na kusoma.

Watoto wametoa wito kwa serikali na washikadau wengine kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao za kushughulikia changamoto zinazowakabili ili kuboresha maisha yao na kulinda mustakabali wao.

Wakati huo huo, wito umetolewa kwa waandalizi wa hafla zinazowahusu watoto kuhakikisha kuwa watoto wanapewa kipaumbele katika shughuli zote zinazopangwa kwa manufaa yao.

Kwa mujibu wa meneja wa programu katika shirika lisilo la kiserikali la SND, Joan Kosgei, ingawa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yalilenga watoto, baadhi yao hawakupata muda wa kutosha kuwasilisha maonyesho waliyojiandaa nayo.

Kosgei amesema suala hilo linaonyesha umuhimu wa waandalizi kuzingatia zaidi ushiriki wa watoto wakati wa kupanga ratiba za hafla kama hizo ili sauti na vipaji vyao vipate nafasi inayostahili.

Post Comment