Highlights

Shirika la PACIDA latoa wito wa maendeleo endelevu na kujitegemea

Na Caroline Waforo

Kuna haja ya kuanzishwa kwa mifumo endelevu ya maendeleo ili kupunguza utegemezi mkubwa wa misaada.

Haya ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la PACIDA, Patrick Katelo, ambaye amesema changamoto za kiusalama zinazoendelea katika Mashariki ya Kati pamoja na kusitishwa kwa misaada kutoka shirika la Marekani la USAID zimeacha pengo kubwa katika juhudi za maendeleo.

Katelo amezungumza wakati wa uzinduzi wa mkakati wa utendakazi wa shirika hilo la PACIDA, wa mwaka 2026 hadi 2030, ambapo amesisitiza umuhimu wa mashirika kuwekeza katika mbinu endelevu za maendeleo zinazojitegemea ili kuhakikisha jamii zinapata suluhu za kudumu.

Wakati huo huo, Naibu Gavana wa kaunti ya Marsabit, Solomon Gubo, amewataka wakaazi wa kaunti hii ya Marsabit kukubali uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi na kuchukua hatua za kukabiliana nayo.

Gubo amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya wakaazi kutotambua athari za mabadiliko ya tabia nchi, hali inayodhoofisha juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wafugaji kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuimarisha mapato.

Shirika la PACIDA limezindua mpango wake wa utendakazi wa miaka mitano wa 2026–2030, unaolenga kuimarisha ustahimilivu na maendeleo endelevu kwa jamii za Kaskazini mwa Kenya na Kusini mwa Ethiopia.

Mkakati huo unalenga kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, elimu, afya na ujenzi wa amani, pamoja na sekta nyingine muhimu za maendeleo.

PACIDA imesema kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia kupunguza utegemezi wa misaada ya dharura huku ukiimarisha uwezo wa jamii kujitegemea na kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi kwa njia endelevu.

Post Comment