Highlights

Washukiwa 9 wa mkasa wa moto katika shule ya utumishi girls wazuiliwa kwa siku 21 zaidi.

Na JB Nateleng

Mahakama ya Naivasha imeamuru wasichana tisa kutoka Shule ya Utumishi Girls Academy iliyoko Gilgil kuzuiliwa katika makao ya watoto ya Nakuru kwa siku 21 ili kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi kuhusu madai ya kuchoma bweni la shule na kusababisha kifo cha wanafunzi 16.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkuu Abdulqadir Ramathan alipuuza ombi la upande wa mashtaka la kuwashikilia kwa siku 30 na kuamuru wazuiliwe kwa siku 21 pekee. Pia alikataa kuwaachilia kwa dhamana au bondi akisema upande wa mashtaka uliwasilisha sababu za msingi za kuendelea kuwazuilia.

Upande wa mashtaka umesema unahitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi, ikiwemo kuwatafuta na kurekodi taarifa za mashahidi muhimu waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, washukiwa walidai walichochewa na mabadiliko ya ratiba ya mitihani, malipo ya shughuli za kitamaduni shuleni na ushawishi kutoka kwa wanafunzi wa shule jirani waliokuwa wamegoma.

Wasichana hao walinaswa kupitia kamera za usalama (CCTV) zikionyesha wakifika katika bweni muda mfupi baada ya saa sita usiku na kudaiwa kuliteketeza kwa moto huku wanafunzi wengine wakiwa wamelala.

Kesi hiyo itatajwa tena Juni 24, 2026.

Post Comment