Wasanii katika Kaunti ya Samburu wafanya matembezi ya amani kuhamasisha kuhusu ugonjwa wa figo
Na Silvio Nangori
Wasanii katika Kaunti ya Samburu wamefanya matembezi ya amani katika mji wa Maralal kwa lengo la kutoa hamasisho kwa wananchi kuhusu ongezeko la visa vya ugonjwa wa figo vinavyoripotiwa katika kaunti hiyo.
Wakiwa na mabango yenye jumbe za kuelimisha umma, wasanii hao walipitia mitaa mbalimbali ya mji huo wakihimiza wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini ugonjwa huo mapema na kupata matibabu kwa wakati.
Wasanii hao wameeleza wasiwasi wao kuhusu idadi inayoongezeka ya wagonjwa wa figo, wakisema kuwa hali hiyo imekuwa mzigo mkubwa kwa familia nyingi kutokana na gharama ya juu ya matibabu na huduma za kusafisha damu (dialysis).
Wametoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Samburu kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza vifaa vya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya figo katika hospitali za umma ili kupunguza gharama wanazobeba wagonjwa wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
Washiriki wa matembezi hayo pia walitaka ushirikiano zaidi kati ya serikali, wahudumu wa afya na viongozi wa jamii katika kuendesha kampeni za uhamasishaji ili kuongeza ufahamu kuhusu visababishi, dalili na mbinu za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.



Post Comment