Madaktari Isiolo waanza mgomo baada ya notisi ya siku 21 kumalizika
Na Silvio Nangori
Madaktari katika Kaunti ya Isiolo wameanza rasmi mgomo kufuatia kumalizika kwa notisi ya siku 21 iliyotolewa na Muungano wa Madaktari KMPDU.
Mgomo huo umeanza rasmi jana usiku wa manane baada ya chama hicho kueleza kuwa Serikali ya Kaunti ya Isiolo imeshindwa kushughulikia changamoto za muda mrefu zinazowakabili wahudumu wa afya.
KMPDU kimesema majaribio ya mara kwa mara ya mazungumzo na uongozi wa kaunti hiyo hayajazaa matunda, hali iliyowalazimu madaktari kusitisha huduma zao.
Miongoni mwa malalamishi yao ni kucheleweshwa kwa mishahara kwa muda wa hadi miezi mitatu, kushindwa kuwasilishwa kwa makato ya kisheria ikiwemo michango ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), pamoja na kutowasilishwa kwa michango ya pensheni kwa miezi kadhaa.
Muungano huo pia kimeeleza kuwepo kwa changamoto ya kupandishwa vyeo kwa madaktari, upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika Hospitali ya Rufaa ya Isiolo Level 5, na mazingira duni ya kazi.



Post Comment