Highlights

Mahakama kuu Marsabit yasitisha kwa muda kutwaliwa kwa matatu na mafuta ya magendo yaliyokamatwa mwezi Juni.

Na Mwandishi Wetu.

Mahakama kuu mjini Marsabit imemuachilia kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi elfu 50 dereva anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha mafuta ya kupikia ambayo hayakuwa yamelipiwa ushuru wala kukaguliwa na shirika la ukaguzi wa ubora wa bidhaa nchini (KEBS), kinyume cha sheria.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Hassan Racho Boru kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya shilingi 300,000, aliyopewa baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha mitungi 180 ya mafuta ya kupikia kutoka Somalia kuingia Kenya kwa kutumia gari la matatu alilokuwa akiendesha.

Boru alikuwa amekiri kosa hilo mbele ya Hakimu Mkuu Edward Oboge.

Hata hivyo, Jaji wa mahakama kuu, Francis Rayola Olel, ameamuru Boru aachiliwe kwa dhamana akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa yake.

Mahakama pia imesitisha kwa muda utekelezaji wa amri ya kutwaliwa kwa gari lililokuwa likisafirisha mafuta hayo pamoja na shehena yenyewe, hadi rufaa hiyo itakaposikilizwa.

Kesi hiyo itatajwa tena Julai 20.

Post Comment