Highlights

Hali ya ukavu kuendelea kutawala Marsabit wiki hii

Na JB Nateleng

Sehemu kubwa ya kaunti ya Marsabit zinatarajiwa kuendelea kushuhudia hali ya ukavu katika kipindi cha kuanzia Julai 14 hadi 20, 2026, kulingana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na idara ya utabiri wa hali ya hewa ya kaunti ya Marsabit.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mvua zitakazonyesha zitakuwa za kiwango kidogo na zinatarajiwa kunyesha katika maeneo machache pekee, yakiwemo mlima Marsabit, Sololo, Hurri Hills pamoja na maeneo ya karibu na Maikona na mpaka wa Ethiopia. Hata hivyo, sehemu kubwa ya maeneo ya tambarare na jangwani yanatarajiwa kubaki makavu katika kipindi chote cha wiki.

Wakati huo huo, maeneo ya nyanda za juu yanatarajiwa kushuhudia hali ya baridi, mawingu, ukungu na umande nyakati za asubuhi, huku maeneo ya tambarare, North Horr na ukanda wa Ziwa Turkana yakitarajiwa kuwa na hali ya joto, ukavu na upepo mkali.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wamehimizwa kutumia kwa uangalifu vyanzo vya maji vilivyopo, huku wafugaji wakitakiwa kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa malisho na maji kwa mifugo yao, hasa katika maeneo ya North Horr, Dukana, Maikona, Turbi, Kargi na maeneo mengine ya chini yanayotegemea ufugaji.

Aidha, wavuvi, waendesha boti na watumiaji wengine wa Ziwa Turkana wameonywa kuwa waangalifu kutokana na upepo mkali unaotarajiwa pamoja na mawimbi makubwa yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Post Comment