Highlights

Washikadau Marsabit wajadiliana hatma ya shule za upili za bweni.

Na Nyabande Orwa

Mchanganuzi wa masuala ya elimu kutoka kaunti ya Marsabit, Profesa Chris Galgalo, amepinga vikali pendekezo la baadhi ya wabunge la kufutilia mbali shule za upili za bweni nchini. Galgalo anasema badala ya kufunga shule hizo, wabunge wanapaswa kuangazia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti mbalimbali za uchunguzi kuhusu migomo na changamoto za wanafunzi shuleni.

Aidha, amewasuta wabunge hao akidai kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha lengo la kuimarisha utaifa kupitia shule za kitaifa na pia kuwaathiri wanafunzi kutoka maeneo ya wafugaji ambao hutegemea shule za bweni ili kuendelea na masomo yao.

Kauli yake inaungwa mkono na mwanaharakati Mohamed Hassan pamoja na Katibu Mkuu wa KUPPET tawi la Marsabit Sarr Galgalo. Wawili hao wanasema badala ya kufutilia mbali shule za bweni, juhudi zinapaswa kuelekezwa katika kuimarisha nidhamu ya wanafunzi kuanzia nyumbani na kuhakikisha mabweni yanazingatia viwango vya usalama vilivyowekwa na wizara ya elimu.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wanaunga mkono wazo la kuwa na shule nyingi za kutwa. Mwenyekiti wa wazazi katika kaunti ya Marsabit Ali Noor anasema mfumo huo utawapa wazazi na walimu nafasi bora ya kufuatilia mienendo ya wanafunzi, kukabiliana na utovu wa nidhamu na kuimarisha usalama wao.

Mjadala huu unajiri siku chache baada ya mkasa wa moto katika shule ya upili ya wasichana ya Utumishi, Gilgil, kaunti ya Nakuru, uliosababisha vifo vya wanafunzi 16.

Post Comment