Ukame na upepo mkali kutarajiwa sehemu kubwa ya Marsabit wiki hii.
Na Nyabande Orwa
Hali ya hewa katika kaunti ya Marsabit inatarajiwa kuwa ya joto na ukame katika maeneo mengi kuanzia tarehe 2 hadi 8 Juni 2026.
Kulingana na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini, maeneo ya Marsabit mjini, Karare, Laisamis, Logologo, Korr, Ngurunit, Turbi, Kargi, South Horr na sehemu kubwa za North Horr yanatarajiwa kubaki bila mvua katika kipindi hicho. Hata hivyo, maeneo machache ya Mlima Marsabit, Sololo, Maikona na yale yanayopakana na Ethiopia yanaweza kushuhudia mvua nyepesi za chini ya milimita tatu.
Maeneo ya nyanda za chini kama vile North Horr, Loiyangalani, Illeret na Maikona yanatarajiwa kushuhudia joto kali la kati ya nyuzi joto 34 hadi 39 mida ya mchana. Wakazi wa Loiyangalani, North Horr, Kargi na maeneo ya mwambao wa Ziwa Turkana wametahadharishwa kuhusu upepo mkali unaoweza kusababisha vumbi na kupunguza uwezo wa kuona.
Wafugaji wanashauriwa kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo kutokana na kuendelea kwa hali ya ukame, huku watumiaji wa Ziwa Turkana wakitakiwa kuwa waangalifu kutokana na mawimbi makubwa yanayoweza kusababishwa na upepo mkali.



Post Comment