Wanasiasa Marsabit waonywa dhidi ya matamshi ya uchochezi.
Na Nyabande Orwa
Huku shughuli za kisiasa zikizidi kushika kasi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, wanasiasa katika kaunti ya Marsabit wametakiwa kuwa waangalifu na matamshi yao ili kuepusha uchochezi na kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Hayo yamesemwa na msaidizi wa kamishna, Martin Buluma. Akizungumza mjini Marsabit, Buluma amesema vyombo vya usalama vinaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya kisiasa na matamshi ya viongozi ili kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani. Amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Marsabit.
Matamshi yake yanajiri wakati tume ya kitaifa ya uwiano na utangamano (NCIC) ikiwataka wanasiasa kote nchini kujiepusha na matamshi ya uchochezi. Mwenyekiti wa tume hiyo, Kepha Omae, amesema maafisa wa NCIC watahudhuria mikutano ya kisiasa ili kufuatilia matamshi ya viongozi na kuhakikisha wanaobainika kukiuka sheria wanachukuliwa hatua za kisheria.



Post Comment