Wafugaji Marsabit wakumbatia mbinu mpya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
ORWA 7PM.
Kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika kaunti ya Marsabit, wafugaji na wakazi wa kaunti hii wameanza kukumbatia njia mbadala za kujipatia kipato na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha mifugo.
Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Indigenous Resource Management Organization (IREMO), Loho Abduba.
Akizungumza na kituo hiki wakati wa warsha ya siku mbili ya mazungumzo ya jamii za wafugaji wa Marsabit, Loho amesema ukame mkali wa miaka ya 2020 hadi 2022 ulisababisha vifo vya maelfu ya mifugo katika maeneo mbalimbali ya kaunti hii, jambo lililowasukuma wafugaji kutafuta mbinu mbadala za kujikinga dhidi ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Loho amesema kwa sasa shirika hilo linashirikiana na jamii mbalimbali kutoa mafunzo kuhusu kilimo katika maeneo yenye mvua za kutosha, hasa maeneo ya milimani. Amesema wakazi pia wanahimizwa kuhifadhi mazao na nyasi baada ya mavuno ili kuhakikisha kunakuwa na akiba ya chakula kwa mifugo wakati wa ukame.
Wakati huo huo, Loho ametoa wito kwa jamii ya Marsabit kuhifadhi mila na desturi zao na kuhakikisha zinapitishwa kwa kizazi cha sasa na kijacho. Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kulinda utamaduni wa jamii mbalimbali za kaunti hiyo usipotee.



Post Comment