Wafugaji Marsabit wahimizwa kujiunga na vyama vya ushirika kuongeza faida.
Na Nyabande Orwa
Mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Centre for Research and Development in Drylands (CRDD), Hussein Wario, amewataka wafugaji kujiunga katika vikundi na vyama vya ushirika ili kuimarisha biashara ya mazao na bidhaa za mifugo, na hivyo kuongeza kipato chao.
Wario aliyasema hayo wakati wa warsha iliyowakutanisha wadau wa sekta ya mifugo pamoja na jamii mbalimbali za kaunti ya Marsabit kujadili njia za kuimarisha sekta hiyo. Amesema kwa muda mrefu wafugaji wamekuwa wakipata hasara kubwa kutokana na ukame unaosababisha vifo vya mifugo, huku wakilazimika kuuza wanyama wao kwa bei ya chini kutokana na ukosefu wa masoko yenye ushindani.
Aidha, Wario amesema warsha kama hizo hutoa fursa kwa wadau kubadilishana mawazo na kutafuta suluhu za changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo. Pia amepongeza kufunguliwa kwa kichinjio cha kisasa cha Isiolo, akisema kitawawezesha wafugaji kuuza nyama iliyoongezwa thamani badala ya mifugo hai, jambo litakalowaongezea mapato.



Post Comment