Bunge la kaunti latakiwa kuongeza mgao wa fedha kwa ufugaji.
Mwakilishi wadi mteule katika bunge la kaunti ya Marsabit ambaye pia ni mwenyekiti wa viongozi wa kina mama, Darare Donje, ametoa wito kwa bunge la kaunti kuongeza mgao wa fedha kwa sekta ya ufugaji ili kuimarisha maendeleo ya sekta hiyo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa kaunti.
Akizungumza wakati wa kongamano la siku mbili la mazungumzo ya jamii ya wafugaji wa Marsabit linaloendelea mjini Marsabit kuanzia leo hadi kesho, Donje amesema sekta ya ufugaji haipaswi kuendelea kudorora kama ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi.
Amesisitiza kuwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hiyo utachangia kuboresha maisha ya wafugaji na kuimarisha uchumi wa kaunti.
Kongamano hilo linajadili masuala ya ufugaji, usimamizi wa maeneo ya malisho (rangelands) na mustakabali wa jamii za wafugaji, sambamba na maadhimisho ya mwaka wa kimataifa wa malisho na wafugaji 2026.
Wakati uo huo, Darare Donje ametoa wito kwa viongozi wa kaunti kuhakikisha kuwa bidhaa zinazotokana na mifugo zinaongezewa thamani ili kuwafaidi wafugaji kiuchumi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha na kuwawezesha wanawake katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mifugo, akisema mchango wao ni muhimu katika kukuza uchumi wa familia na maendeleo ya jamii.



Post Comment