Maeneo mengi ya Marsabit kubaki makavu, Maikona na maeneo ya mpakani yakitarajiwa kupata mvua nyepesi
Na Samuel Kosgei
Kaunti ya Marsabit inatarajiwa kushuhudia hali ya hewa ya ukavu katika maeneo mengi kuanzia leo tarehe 28 Julai hadi 3 Agosti 2026 huku msimu wa baridi na ukavu ukiendelea kutawala kaskazini mwa Kenya.
Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, manyunyu kiasi zinatarajiwa katika maeneo machache ya milimani ikiwemo Mlima Marsabit, Nyanda za Juu za Sololo, Hurri Hills pamoja na maeneo ya karibu na Maikona na mpakani mwa Ethiopia.
Utabiri unasema kuwa Maikona huenda ikapokea mvua kiasi, kati ya milimita 1 hadi 1.5, huku maeneo ya Sololo, Butiye, Obbu, Manyatta na Jaldesa yakitarajiwa kupata mvua nyepesi ya chini ya milimita moja.
Maeneo mengi ya tambarare, North Horr, Loiyangalani, Turbi, Laisamis na Bonde la Ziwa Turkana yanatarajiwa kubaki makavu katika kipindi chote cha utabiri.
Maeneo ya nyanda za juu yanatarajiwa kushuhudia asubuhi za baridi zenye mawingu na ukungu wa hapa na pale, huku maeneo ya tambarare na Bonde la Ziwa Turkana yakitarajiwa kuendelea kuwa na hali ya joto, ukavu na upepo wa wastani hadi mkali wakati mwingine.
Wakazi wanashauriwa kuendelea kuhifadhi maji na wafugaji kufuatilia kwa karibu hali ya malisho na vyanzo vya maji hususan katika maeneo ya North Horr, Dukana, Maikona, Turbi na Kargi.



Post Comment