Highlights

Ushirikiano wa serikali ya kaunti na wadau wakuza elimu na ujuzi.

Na Joyce Akinyi

Ushirikiano kati ya serikali ya kaunti ya Marsabit na mashirika yasiyo ya kiserikali umeelezwa kuwa muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu na kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa madarasa matatu mapya na gari la mafunzo katika chuo cha ufundi cha Saku, meneja wa kitaifa wa shirika la Catholic Relief Services CRS, Margaret Kaiga, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo, akibainisha kuwa umesaidia kuimarisha utoaji wa huduma za ushauri nasaha kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi kote kaunti ya Marsabit.

Kaiga amesema ni wajibu wa kila mdau katika sekta ya elimu kushirikiana ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua maisha ya wanafunzi pamoja na walimu.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa wakfu wa kampuni moja ya mawasiliano, Joe Ogutu, amewataka wanafunzi kuwa waaminifu, wenye nidhamu na kujituma katika masomo yao akisema kupata ujuzi wa kutosha kutawawezesha kujiboresha, kujiajiri na kufanikisha malengo yao ya baadaye.

Post Comment