Highlights

Vijana Marsabit wahimizwa kuepuka kushawishiwa kujiunga na makundi ya kigaidi

Na Silvio Nangori

Vijana katika Kaunti ya Marsabit wamehimizwa kuwa macho na kujiepusha na ushawishi wa kujiunga na makundi ya kigaidi na badala yake kuwa mabalozi wa amani, maendeleo na mshikamano katika jamii.

Akizungumza na Shajara ya Jangwani katika warsha iliyofanyika mjini Marsabit, Afisa Mkuu wa mahusiano katika Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC), Joseph Kanyiri, amewataka vijana kukataa kuhusishwa na shughuli zozote zinazoweza kuwavuta kujiunga na makundi haramu.

Kulingana na Kanyiri baadhi ya makundi ya kigaidi hutumia mitandao ya kijamii kuwashawishi vijana, hivyo kuwataka kuitumia teknolojia hiyo kwa njia chanya kwa ajili ya elimu, maendeleo binafsi na kujenga mustakabali wao wenyewe.

Wakati huo huo, mtetezi wa haki za binadamu na Mkurugenzi wa Shirika la MWADO, Nuria Gollo, amesema ukosefu wa ajira ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma baadhi ya vijana kujiunga na makundi haramu na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Amesema changamoto hiyo inaendelea kuathiri vijana wengi katika Kaunti ya Marsabit na kwamba kuna haja ya kuimarisha fursa za kiuchumi ili kuwakinga dhidi ya ushawishi wa makundi haramu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Initiative for Progressive Change (IFPC), Hassan Mulata, amesema vijana Marsabit wamepewa kipaumbele katika shughuli za uhamasishaji ili kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika maendeleo ya kijamii.

Warsha hiyo iliandaliwa na Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC) kupitia mpango unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya unaolenga kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya usalama katika kukabiliana na vitisho vya usalama.

Warsha hiyo iliwaleta pamoja wawakilishi wa jamii, maafisa wa serikali, vyombo vya usalama na wadau mbalimbali kujadili na kuandaa mikakati ya kukabiliana na vitisho vya ugaidi na misimamo mikali ya vurugu katika ngazi ya jamii.

Post Comment