Highlights

Wanaskauti Marsabit wakongamana Moyale kwa mafunzo na mashindano.

Na JB Nateleng

Zaidi ya wanaskauti 300 kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti ya Marsabit wamekusanyika mjini Moyale kwa ajili ya mafunzo, mashindano na shughuli za kujenga uwezo kupitia kongamano la wanaskauti lililoandaliwa na viongozi wa uskauti Marsabit.

Akizungumza na idhaa hii, Kamishna wa wanaskauti kaunti ya Marsabit, John Pope Wambisa, amesema lengo la kongamano hilo ni kuimarisha shughuli za uskauti katika eneo la Moyale na kuwapa wanaskauti nafasi ya kuchagua viongozi watakaosaidia kuendeleza programu za uskauti katika eneo hilo.

Naye mtathmini wa kongamano hilo, Caroline Atieno Oyugi, amesema shughuli za uskauti zina manufaa makubwa kwa watoto wa kike kwa sababu inawapa maarifa, stadi za maisha na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Atieno pia amewataka wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika warsha na kongamano kama hilo ili waweze kujifunza, kushirikiana na wenzao kutoka jamii tofauti na kukuza maadili, tamaduni na uelewano wa kijamii.

Kwa upande wake, Ali Abdi ambaye pia ni mtathmini wa kongamano hilo, amesema wanaskauti wana mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano akibainisha kuwa kongamano hilo limewapa washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Marsabit fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya uskauti.

Post Comment