Highlights

Mashindano ya michezo ya muhula wa pili katika kaunti ya Marsabit yaanza rasmi hii leo.

Na JB Nateleng

Mashindano ya michezo ya muhula wa pili kwa shule za upili ngazi ya kaunti yameanza rasmi leo katika kaunti ya Marsabit yakizikutanisha shule zilizofuzu kutoka kaunti ndogo zote jimboni.

Mashindano hayo yanajumuisha kandanda, raga, voliboli na mpira wa kikapu, huku yakilenga kutafuta timu zitakazoiwakilisha kaunti katika kitengo cha mkoa wa mashariki ambayo yataandaliwa wiki ijayo katika kaunti ya Makueni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Mwenyekiti wa michezo wa shule za sekondari kaunti ya Marsabit na mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Dakabaricha, Ibrahim Gere, amewataka wanafunzi kuzingatia michezo ya kiungwana, kuheshimiana na kutumia mashindano hayo kujenga urafiki na mshikamano.

Naye mwenyekiti wa chama cha wakuu wa shule za sekondari nchini (KESSHA) tawi la Marsabit na mwalimu mkuu wa Moi Girls Marsabit, Halima Adan, amewahimiza wanafunzi kudumisha nidhamu ya hali ya juu ili kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa amani na mafanikio.

Viongozi hao pia wamewataka walimu kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki michezoni kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa wakionya kuwa shule yoyote itakayobainika kumtumia mchezaji ambaye si mwanafunzi wa shule hiyo au aliyepita umri unaoruhusiwa itachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwemo kupigwa marufuku kushiriki mashindano hayo.

Mashindano hayo yanatarajiwa kutamatika tarehe 4 Julai 2026 na timu ambayo itaibuka na ushindi itawakilisha kaunti ya Marsabit kwenye mashindano ya mkoa wa mashariki ambayo yataandaliwa katika kaunti ya Makueni kuanzia tarehe 8 Julai 2026 hadi 11 Julai 2026

Post Comment