Kaunti ya Marsabit yatarajiwa kushuhudia viwango tofauti vya mvua
Na Samuel Kosgei
Kaunti ya Marsabit inatarajiwa kushuhudia viwango tofauti vya mvua kuanzia leo Aprili 28 hadi Mei 4, huku baadhi ya maeneo yakipokea mvua kubwa na mengine yakisalia makavu.
Katika maeneo ya Marsabit Town, Sagante/Jaldesa na Karare yaliyo chini ya Marsabit Central, mvua ya wastani hadi kubwa inatarajiwa kunyesha wiki nzima. Maeneo ya Mlima Marsabit huenda yakapokea mvua zaidi. Hali hii inaweza kusababisha mafuriko katika maeneo ya chini.
Katika eneo la North Horr na Dukana, mvua nyepesi hadi wastani inatarajiwa kunyesha, huku baadhi ya maeneo yakipokea hadi milimita 68. Dukana inatarajiwa kuwa na unyevunyevu zaidi kuliko sehemu za ndani ya North Horr. Kutokana na hali hiyo, malisho yanatarajiwa kuimarika katika baadhi ya maeneo.
Eneo la Laisamis, ikiwemo Logologo, Korr na Ngurunit, linatarajiwa kupata mvua za viwango tofauti. Logologo na Korr zinatarajiwa kupokea mvua zaidi huku maeneo ya ndani ya Laisamis yakisalia na mvua kidogo.
Katika kaunti ndogo ya Moyale pamoja na Sololo, Uran, Obbu na Butiye, mvua kubwa zaidi kaunti nzima inatarajiwa kunyesha. Ukanda wa mpakani mwa Ethiopia unatarajiwa kushuhudia dhoruba kali pamoja na hatari ya mafuriko, huku mvua hizo zikisaidia malisho na kujaza vyanzo vya maji.
Turbi na maeneo ya jirani yanatarajiwa kupokea mvua ya wastani, hali itakayofaa mifugo na ukuaji wa mimea.
Eneo la Loiyangalani karibu na Ziwa Turkana linatarajiwa kubaki mkavu, huku hali ya joto na ukame ikiendelea bila nafuu kubwa kwa malisho.
Katika maeneo ya Kargi na South Horr, mvua nyepesi ya hapa na pale inatarajiwa. Maeneo mengi yataendelea kuwa makavu ingawa baadhi yanaweza kupata nafuu kidogo.



Post Comment